Wadakwa kwa kifo cha aliyejinyonga mtini


Tabora. Watu watano wanashikiliwa na polisi baada ya mtu kukutwa amejinyonga mtini muda mfupi baada ya kutoka katika sherehe mjini Tabora.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Issa amesema watu hao wanashikiliwa kutokana na mtu aliyetambuliwa kwa jina moja la Musa kukutwa amejinyonga kwenye tawi la mti.

Mmoja wa watu waliokuwa katika sherehe iliyohudhuriwa na Musa ambaye hakupenda jina lake litajwe amesema kulikuwa na mabishano na kutolewana kati yake na baadhi ya watu na baadaye walitoweka.

“Niliwaona wakitoleana maneno, lakini sikujua mwisho wake kwa vile niliendelea na kufuatilia sherehe na kushtushwa kesho yake Musa kuonekana amejinyonga,” amesema.

Mkazi wa mjini hapa, Yassin Maulid amesema kwa namna alivyouona mwili wa Musa anahisi kuna mkono wa mtu umehusika kwa vile alikuwa akitokwa damu katika baadhi ya sehemu za mwili wake.

Kamanda Issa amesema mazingira yaliyokuwapo kutokana na uchunguzi wa awali yanaonyesha kwamba mtu huyo aliuawa kisha kutundikwa kwenye mti ili kupoteza ushahidi.

“Marehemu alikutwa na michubuko pamoja na damu na kwa uchunguzi wetu wa awali kuna watu wanahusika na kifo cha mtu huyu,” amesema Kamanda Issa.

Ameongeza kuwa watu hao wanahojiwa na polisi kwa kuwa inaelezwa kabla ya kifo, Musa aligombana na baadhi yao wakati wa mkesha wa sherehe mwishoni mwa wiki na kesho yake kuonekana amejinyonga.

Kamanda ametoa onyo kwa watu wanaofanya uhalifu kwa kisingizio cha aina yoyote kuwa jeshi hilo liko imara na litawabaini, huku akiwataka wananchi wasijihusishe na uhalifu.