Wadakwa na misokoto 1,082 ya bangi

Moshi. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watuhumiwa wawili kwa tuhuma za kukutwa na bangi misokoto 1,082.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Wilibroad Mutafungwa amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao  ni kutokana na misako mikali inayoendelea kufanywa na jeshi hilo na kufanikisha upatikanaji wa wahalifu wanaovunja Sheria.

"Juhudi zinazofanywa na jeshi la Polisi kwa kufanya doria katika baadhi ya maeneo ya Moshi Mjini imefanikisha kukamata wahalifu wanaovunja sheria," amesema.

Pia amesema tukio hilo lilitokea jana katika eneo la Shaurimoyo, Wilaya ya Moshi na polisi waliwafuatilia watuhumiwa hao hadi wanapoishi na kufanya upekuzi ambao ulifanikiwa kuwakuta na kiasi cha bangi misokoto iliyohifadhiwa ndani ya begi lao.