Wajisaidia vichakani kwa miaka miwili

Katavi.Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Usevya wilayani Mlele mkoani Katavi, wanalazimika kujisaidia vichakani baada ya kukosa vyoo kwa zaidi ya miaka miwili.

Sekondari hiyo inayomilikiwa na Kata ya Usevya, ina madarasa pia ya kidato cha tano na sita na ina upungufu wa matundu 35 ya vyoo baada ya manne ya awali kujaa.

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tano shuleni hapo, Juniour Mgallah na Moshi Ramadhani, wamesema hulazimika kutumia muda mwingi kutafuta vichaka vya kwenda kujisaidia.

Akizungumza na vyombo vya habari, Mkuu wa shule hiyo, Denis Thilia amekiri kuwapo kwa tatizo hilo sambamba na upungufu wa mabweni matatu ya wanafunzi wa kike.

Anasema ameshatoa taarifa serikalini lakini bado jitihada za kumaliza matatizo hayo hazijafanyika.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe, Erasto Kiwale, amesema taarifa hizo anazo na ofisi yake imeshaanza kuzifanyia kazi kwa kuwaagiza watendaji wa kijiji na kata kulishughurika mara moja.