Walimu wakuu 25 Mpwapwa washushwa vyeo

Dar es Salaam.  Zaidi ya walimu wakuu 25 wa shule za msingi Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, wamevuliwa vyeo vyao na kuwa walimu wa kawaida kutokana na usimamizi mbovu huku wengine 55 wakihamishwa shule za pembezoni ili kuinua kiwango cha elimu wilayani humo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpwapwa, Mohamed Maje amesema hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya harambee kwa wakazi wa wilaya hiyo wanaoishi Dar es Salaam kuchangia madawati.

Katika harambee hiyo, wanatarajiwa kupata Sh587 milioni.
Maje amesema walimu wakuu hao walishindwa kusimamia maudhurio ya walimu kuingia darasani na ukamilishaji wa silabasi jambo ambalo limesababisha wilaya hiyo kimkoa kuwa ya mwisho..

Amesema Januari 27 mwaka huu halmashauri hiyo ilikaa na kukubaliana kuwa idara ya elimu ikague shule hizo ili kuangalia sababu ya kushuka elimu katika wilaya hiyo.

“Sababu iliyochangia kushuka kwa elimu katika wilaya yetu walimu wakuu wameshindwa kusimamia ipasavyo, tumegundua walimu walikuwa hawaingii darasani matokeo yake hawakukamilisha silabasi za masomo,” amesema Maje.