MAELFU ya mashabiki wa Muziki wa Kizazi Kipya nchini walikuwa wameelekeza macho na masikio yao katika Ukumbi wa Barcklays Center pale New York, Marekani kwenye utoaji wa tuzo za BET, ambako Mtanzania Diamond Platnumz alikuwa mmoja wa wasanii saba kutoka Afrika waliokuwa wakishindana kuwania kipengele cha Best Internatinal Act 2016 (Africa).
Wakitaraji kuwa mwakilishi wao huyo angeibuka kinara, ghafla ikatangazwa kuwa DJ Black Coffee kutoka Afrika Kusini, ndiye mshindi na hivyo kufuta ndoto za Diamond kutwaa tuzo katika ardhi ya Marekani. Mshindi huyu ni nani?
Jina lake linaweza kuwa geni kwa baadhi, lakini kwa wafuatiliaji wa burudani watakuwa wanamfahamu vyema mkali huyu wa miondoko ya House ambaye pia ni prodyuza hasa kupitia ngoma yake iitwayo Juju, iliyofanya vizuri sana barani Afrika miaka ya hivi karibuni.
Ni mzaliwa wa jijini Durban akiitwa Nkosinathi Innocent Maphumulo, lakini alipogusa tu ulimwengu wa ‘entertainment’ mwanzoni mwa miaka ya 1990, akajiita DJ Black Coffee.
Ameanzia wapi muziki?
Dj Black Coffee kabla ya kuufanya muziki kuwa biashara ya kumuingizia mkwanja, alikuwa ni mwanakwaya katika shule yake ya sekondari, baadaye alikwenda kusomea muziki katika chuo kiitwacho Natal Technikon na kabla ya kumaliza masomo, alianzisha bendi iitwayo Shana (Simply Hot And Naturally African).Akiwa ameanza kuvuna mashabiki kutokana na kazi yake ya muziki, mwaka 2003 mkali huyo alikuwa mmoja kati ya wanamuziki wawili wa Afrika Kusini waliochaguliwa na kituo cha kujifunzia muziki kiitwacho The Red Bull Music Academy kuwa Dj wake, ambapo huo ndiyo ukawa mwanzo wa kujipatia umaarufu kupitia muziki na u-dj.
Mpaka sasa amefanikiwa kutoa albamu sita ambazo ni Black Coffee (2005), Have Another One (2007), Home Brewed (2009), Africa Rising DVD (2012), Africa Rising CD (2012) pamoja na Pieces Af Me ya mwaka 2015 na albamu zote hizo zimefanya vizuri kimauzo.
Moja ya vitu vilivyompa umaarufu mkali huyu na kumtofautisha na wasanii wengi ni uwezo wake wa kucheza na vyombo vya muziki kwa kutumia mkono wake mmoja tu wa kushoto kwani akiwa na miaka 13 alipoteza matumizi ya mkono wake wa kulia baada ya kupata ajali ya kugongwa na gari katika sherehe za kuachiwa huru kwa hayati Nelson Mandela.
Mwaka 2010 alivunja rekodi ya dunia kwa kuwa Dj mwenye uwezo wa kuburudisha kwa muda mrefu akitumia mkono mmoja tu. Anatajwa pia kuwa ni mmoja kati ya wasanii wanaopendwa mno Afrika Kusini, hasa kwa msaada wake kwa jamii ikikumbukwa mwaka 2009, aligawa asilimia tano ya mauzo ya albamu zake zote kwa makundi maalumu yenye uhitaji.
Ukongwe umempiga tafu!
Katika orodha ya wasanii waliokuwa wanachuana kuwania tuzo ya BET katika kipengele cha Best International Act 2106 (Africa) ambao ni Wizkid, AKA, Diamond Platnumz, Cassper Nyovest, Yemi Alade na Serge Beynaud, ni DJ Black Coffee pekee ambaye ni mkongwe kuliko wote na mwenye mafanikio kwenye tasnia ya muziki.
Tuzo ya mwaka huu kwake ni ya 16 ikiwemo ile ya Channel O aliyobeba mwaka 2011 ya msanii mwenye kipaji zaidi kuliko wote Afrika.
Kuhusu familia
Mwaka 2011 alifunga ndoa na muigizaji mwenye jina kubwa Afrika Kusini, Mbali Mlotswa na wamefanikiwa kupata watoto wawili, Anesu na Asante lakini kabla ya hapo, DJ Black Coffee alikuwa na watoto wengine wawili aliowapa katika uhusiano wake wa nje ambao ni Esona na Lilitha.