Omog kuwasili leo, kusaini kuifundisha Simba SC

Kocha raia wa Cameroon Joseph Marius Omog

Kocha raia wa Cameroon Joseph Marius Omog anatarajiwa kuwasili usiku wa leo kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho na uongozi wa Simba kabla ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha klabu hiyo.

Omog na Simba SC wamefikia makubaliano baada ya mazungumzo ya awali na Mcameroon huyo ambaye amekubali kuja kusaini mkataba Dar es Salaam baada ya kutumiwa tiketi.

Simba itakuwa klabu ya pili kwa Omog kufundisha Tanzania baada ya awali kuwa na Azam FC, aliyoiongoza kwa msimu mmoja na nusu ikishinda mechi 30 kati ya 55 za mashindano yote, sare 14 na kufungwa mara 11.

Mwalimu huyo aliyeipa Leopard FC ya Kongo Brazaville Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2014, enzi zake alichezea Yaounde na ni mwalimu wa kiwango cha juu cha ufundishaji soka na mazoezi ya viungo aliyehitimu vizuri mafunzo yake katika Chuo cha Vijana na Michezo, mjini Yaounde, Cameroon.