Sukari bado tatizo nchini - Majaliwa

Serikali imesema licha ya kuingiza tani nyingi za sukari nchi lakini bado kuna tatizo la sukari katika baadhi ya maeneo ya katika makao makuu za mikoa na wilaya kwa kuuzwa bei ya juu kuliko bei elekezi kwa hisia za kuwa bidhaa hiyo imeadimika nchini.

Akizungumza wakati wa kuahirisha Bunge la 11 hii leo, Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, amesema kuwa hadi kufikia Juni 30 kiasi cha tani elfu 63 za sukari zimeingizwa kati ya tani elfu 80 zilizokuwa zinahitajika kufidia pengo lililopo.

Mhe. Majaliwa amesema njia pekee ya kuondokana na uhabari wa sukari uliokuwepo miaka yote ni kuongeza uzalishaji wa sukari ya ndani kwa kukamilisha mpango makakati wa maendeleo ya sukari kwa miaka mitano ijayo.

Mhe. Majaliwa amesema kuwa serikali itaendelea kusimamia soko la sukari kuendelea kushuka ili mlaji wa chini amudu kununua huku ikifanya tathmini ya mahitaji halisi ya sukari nchini kutokana kuingiza kiasi kingi cha sukari lakini bado kumeonekana na upungufu mkubwa.

Waziri Majaliwa amesema moja kati ya Malengo yaliyopo katika mpango huo ni pamoja na kuanzisha kwa viwanda vipya ambapo vitaanzishwa viwanda vya kati vitatu pamoja na kuanzisha viwanda vikubeas katika maeneo ya Bagamoyo, Rufiji, Kigoma na Kidunda.

Aidha wataongeza tija ya uzalishaji wa miwa inayolimwa na wakulima wadogo, kwa kuboresha upatikanaji wa pembejeo, miundombinu ya umwagiliaji, na kuboresha mfumo wa uendeshaji wa vyama vya wakulima wa miwa.