Ahadi ya Rais Magufuli inayolenga kuboresha miundombinu Mwanza iweze kufanana na (Geneva) Uswiss

Katika kutekeleza moja kati ya ahadi za Rais Dk. John Pombe Magufuli, zinazolenga kuboresha miundombinu ya Jiji la Mwanza iweze kufanana na (Geneva) mji mkuu wa Uswiss,

 Serikali inatarajia kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 541.34, kama utekelezaji wa ahadi hiyo.
Miongoni mwa barabara zitakazohusishwa na ujenzi huo utakaogharimu shilingi millioni 625,198, 238, ni ile itokayo eneo la sabasaba kata ya Ilemela hadi Buswelu, ikiwemo inayotoka Nyakato na kisha kuungana na barabara ya Buswelu.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini hapa wakati wa ziara ya ukaguzi wa barabara hizo, Mbunge wa Jimbo la Ilemela, ambaye pia ni Naibu Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula, amesema ujenzi huo utakamilika kabla ya miaka mitano.

Katika mkakati huo unaolenga kuboresha huduma za Wananchi, vilevile Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Jijini la Mwanza imeanza kuzifanyia ukarabati barabara zake, baada ya kupokea fedha kutoka Serikali kuu kwa ajili ya matengenezo ya dharula.

Kutokana mikakati hiyo Wananchi wa maeneo mbalimbali yaliyoanza kunufaika na ukarabati huo pamoja na Diwani wa kata ya Kirumba Alex Ngussa, wameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma hizo, zitakazowezesha barabara zisizopitika kupitika kwa urahisi.