Dangote Ashuka Matajiri Bora 100 Duniani

DANGOTE
Tajiri namba moja barani Afrika Aliko Dangote.

Tajiri namba moja barani Afrika Aliko Dangote, sasa anashika nafasi ya 104 kati ya matajiri duniani. Dangote ameshuka kwa mara ya kwanza kati ya matajiri bora 100 chini ya jua kwa mujibu wa mtandao wa Bloomberg billionaires ranking.

Bloomberg wamesema kwamba Dangote ameshuka sababu kubwa ikiwa ni kuporomoka kwa thamani ya pesa ya nchi ya Nigeria, Naira. Ambayo imeshuka kutoka 198 hadi 300, na inakadiriwa kupunguza karibu robo ya utajiri wa Dangote ambaye bado anawekeza vitega uchumi mbalimbali katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania.

Kulingana na ripoti hiyo ya Bloomberg billionaires, Dangote, aliyekuwa na utajiri wa dola za Marekani $15.4 billioni (Naira 3.05 trilioni) mwezi Machi mwaka huu mpaka sasa anamiliki utajiri unaofikia dola za Marekani bilioni 11.1 (Naira3.3 trillion), kwa maana tajiri kwa pesa za nchini kwao lakini maskini kwa pesa za dola ya Marekani.

Pamoja na kushuka kwake lakini bado kawazidi mabilionea wenye majina makubwa akiwemo mgombea uraisi wa Marekani, Donald Trump ($4.5) na msanii Oprah Winfrey ($3.1), anayetajwa kama mwanamke wa pili kwa utajiri duniani.

Kulingana na Jarida la Forbes la mwezi Juni 2015 ‘The World’s Billionaire’ rankings, mfanyabiashara huyo anamiliki utajiri unaokadiriwa kufikia $12.7 billion dollars na alikuwa akishika nafasi ya 51 miongoni mwa matajiri duniani na nafasi 71 ya watu wenye nguvu duniani.