Kipaombele changu sasa siyo uchaguzi ujao - Bulaya

Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini kupitia tiketi ya CHADEMA Ester Bulaya amesema kipaombele chake kwa sasa siyo uchaguzi ujao wa 2020, bali ni kuwatumikia wananchi wa jimbo lake na kutimiza ahadi zake.

Bulaya pia amesema kuwa wananchi wa jimbo lake watampima kutokana na namna anavyofanya kazi za kuwatumikia kulingana na ahadi ambazo aliahidi.

Akizungumza katika kipindi cha HOTMIX kinachorushwa na EATV, Bulaya amesema mara baada ya kuchaguliwa na wananchi wa Bunda ameweza kusaidia mchakato wa kutatua kero mbalimbali za wananchi kama ujenzi wa zahanati, ujenzi wa bweni, ujenzi wa madarasa, miradi ya maji, madawati mashuleni pamoja na kugawa vifaa vya michezo kwa vijana ili waweze kushiriki michezo.

“Jimbo langu lina changamoto kubwa sana za huduma za kijamiii, nimeanza kukabiliana nazo kwa kuhakikisha kila senti tunayopata kwa ajili ya maendeleo inatumika kama ilivyokusudiwa, na katika ubunge wangu mara nyingi ninashinda jimboni ili kuhudumia wananchi kama nilivyoahidi” Amesema Bulaya.

Aidha ameongeza kuwa kati ya mambo aliyoahidi wananchi ni kuwa mtumishi na siyo kuwa mtawala, hivyo kwa kufanya hivyo anaamini wananchi watampima kutokana na namna anavyotatua kero za wananchi.

Pamoja na hayo ameongeza kuwa wananchi wengi walikuwa hawana uelewa juu ya mfuko wa jimbo, ila yeye amefanikiwa kutumia mfuko wa jimbo kwa kusaidiana na wajumbe wa mfuko huo katika kutatua kero za wananchi katika maeneo mbalimbali ya jimbo lake.

“Pesa za mfuko wa jimbo hutofautiana kutoka jimbo moja hadi lingine, hivyo kwa upande wangu pesa ambazo nimepata nimeanza kuzitumia kukarabati miradi mbalimbali na jambo hili linawajengea wananchi imani kubwa juu ya matumizi ya fedha hizo na dhana ya ushirikishwaji wa mambo yanayowahusu” Amesisitiza Bulaya.