Mabasi yenye kasoro yapewa siku 7 kurekebishwa

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imetoa siku saba kwa wamiliki wa mabasi yote ambayo yaligundulika yanakasoro wakati wa ukaguzi ili waweze kuendelea na usafirishaji kama ilivyokua awali.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, meneja wa mawasiliano wa SUMATRA, Bw. David Mziray amesema kuwa wamekubaliana na wamiliki hao kuendelea na ukaguzi wa vyombo hivyo vya moto kama ilivyokuwa awali bila kuathiri upande wowote wa abiria au wamiliki hao wa mabasi.

Mziray amesema kuwa SUMATRA wataendelea kufungia mabasi ya kampuni yatakayoonekana mabovu na yale yatakayokuwa yanasababisha ajali za mara kwa mara ili kulinda usalama wa raia na kuepusha vifo au majeruhi yanayoweza kuepukika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafari wa Barabara Johansen Kahatano amesema kuwa wataendelea na ukaguzi wao kama ilivyokuwa awali ikiwemo ule wa kushtukiza ili kuwabaini wanaokiuka leseni za usafirishaji ili sheria ichukue mkondo wake.

Kahatano amesema kuwa ukaguzi huo wa kushtukiza umesaidia sana baada ya kubaini magari mengi zaidi kuwa ni mabovu na yanaendelea kufanya biashara ya usafirishaji abiria nchini.