Mtoto aieleza mahakama alivyolazimishwa kuolewa

Dar es Salaam.  Shahidi wa kwanza katika kesi ya kubaka na kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha tatu (16), inayomkabili mwalimu wa madrasa Khalifa Chubwa (26), ameileza mahakama jinsi alivyolazimishwa kufunga ndoa.

Shahidi huyo ambaye ni mlalamikaji katika kesi hiyo, ameieleza  Mahakama ya Wilaya ya Ilala kuwa mshtakiwa alimshawishi aache shule ili amuoe na kisha ampeleke Zanzibar akamfundishe kushona nguo.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Sylvia Mitando, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Said Mkasiwa, shahidi huyo alidai alikuwa akiishi na mama yake mdogo aliyekuwa mke wa Chubwa kabla ya kutalikiana.

“Baada ya mama mdogo kuondoka, Chubwa alinishawishi niache shule kwa madai kuwa elimu ya dunia haina faida,” alidai.

Alieleza kuwa baada ya kuacha masomo hayo, walifunga ndoa kwa siri.