F Mwanamke abakwa na kuuawa Dodoma | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mwanamke abakwa na kuuawa Dodoma

Mwanamke mmoja ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 mkazi wa kijiji cha Iringa Mvumi kata ya mvumi Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma amekutwa amefariki dunia na kutupwa kichakani baada ya kubakwa na watu wasiofahamika.

Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa amesema kuwa tukio hilo limetokea Agosti 10 mwaka huu majira ya saa saba na nusu mchana katika kata ya Mvumi Wilayani Chamwino.

Mambosasa amesema kuwa mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi zaidi na msako wa watu waliotenda uhalifu huo unaendelea ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Katika tukio lingine mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Mkengela Mchechele, mkazi wa kijiji cha Mlali-Iyengu Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani na kuchapwa viboko 12 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 11 (jina linahifadhiwa).

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi wa Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kongwa, Mary Senapee ameamuru pia mhalifu huyo kulipa faini ya shilingi milioni moja pindi atakapotoka gerezani ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Kabla ya kusomwa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kandoro Babile ameieleza mahakama kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Machi 29 mwaka huu katika kijiji cha Malali-Iyengu baada ya kumkamata kwa nguvu mtoto huyo akiwa nyumbani kwake.

Aidha Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma alisema, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limejipanga vizuri kuhakikisha wahalifu wote wanaotenda makosa wanakamatwa, upelelezi wa kina unafanyika ipasavyo kwa mujibu wa sheria na kuwafikisha mahakamani ili haki iweze kutendeka.