Nyimbo za uzalendo zifundishwe shuleni: Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Prof. Joyce Ndalichako amewataka vijana wanaohitimu mafunzo ya ukuruta kuyatumia vizuri katika kutunza amani na usalama wa nchi.

Akizungumza na vijana 1577 ambao walihitimu kidato cha sita na kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kambi ya Ruvu mkoa wa Pwani, Ndalichako amesisitiza utii wa sheria za nchi na kulinda amani ya nchi.

“Tusikubali kupandikizwa mbegu ya chuki miongoni mwetu, kwa sababu watanzania tumejengewa upendo na mshikamano, tujitahidi kulinda amani yetu, na mafunzo mliyopatiwa yawasaidie katika maeneo yenu na siyo kuyatumia kwa kufanya mambo yenye uchochezi na kusahau uzalendo” Amesema Ndalichako.

Aidha Waziri Ndalichako amewataka maafisa elimu nchini kuhakikisha nyimbo za uzalendo zinafundishwa katika shule za msingi na wanafunzi waimbe nyimbo hizo ili waweze kutambua kwamba uzalendo ni jambo muhimu katika nchi yetu.