Tozo kubwa ni kero kwenye masoko - Simbachawene

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. George Simbachawene amesema moja kati ya changamoto zinazojitokeza kwenye masoko ya uwekezaji ni kutokana na kupangwa kwa tozo kubwa ya upangaji katika masoko mbalimbali

Waziri Simbachawene ameyasema hayo kwenye mahojiano maalum na East Africa Radio kuhusu taratibu zilizopo ambazo zinapaswa kutumika katika ulipaji ushuru kwa wafanyabiashara wadogo kwenye masoko mbalimbali nchini.

Amesema swala la kutenga maeneo kwaajili ya shughuli za masoko ni moja ya mambo muhimu yanayozingatiwa na serikali, hivyo halmashauri za majiji, manispaa na miji vitoe kipaumbele kwakuwa ni sehemu muhimu za kutoa huduma na kufanya biashara.

Ameongeza kuwa ushuru wa biashara kwenye masoko hayo yalenge katika kuboresha miundombinu ya soko hilo na kuzitaka mamlaka husika wasimamie ushuru wanaokusanya kwenye masoko hayo yaende kwenye matumizi ya kusimamia soko liwe bora zaidi na wasibadilishe matumizi ya pesa hizo.