Tunadanganya mashabiki kwa ku'fake' maisha: Kassim

Msanii Kassim Mganga amefunguka juu ya tabia za baadhi ya wasanii kuwadanganya mashabiki pale wanapoonesha vitu vya thamani, ambavyo havina ukweli kuwa wanavimiliki.

Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East AFrica Radio, Kassim Mganga amesema wasanii wengi wa bongo wanaigiza maisha ili kuwadanganya watu, na kujilinganisha na wasanii wa Marekani ambao hizo mali zinakuwa ni zao kweli.

"Mi ambacho nimejifunza, wenzetu hawa'act, wenzetu wako real, ndio maisha yako vile, ukimuona Chris Brown au ukimuona 50 Cent pamoja na umri wake aliokuwa nao leo, anaonesha magari yake na nini na nini, watu wapo kwenye ushindani wa biashara kubwa sana, kwa hiyo anachokifanya kina mantiki, sisi tumekuwa tuna'fake vitu vingi havipo real, lakini tunataka tuwaoneshe kwenye mitandao, tunadanganya, tunawadanganya sana mashabiki wetu, mashabiki wanatuona si watu ambao tuna maisha makubwa sana, wakati haiko hivyo kiuhalisia", alisema Kassim Mganga.

Kassim aliendelea kusema kuwa kitendo hicho si kizuri hasa kwa wasanii wachanga, ingawa hakuna mtu anayekatazwa ku'post kitu kwenye mitandao ya kijamii.

"Wadogo zetu wamekuwa wako hivyo na haikatazwi, unajua huwezi kumkataza mtu na makuzi yake na maamuzi yake, maisha ya kwake, uongo wa kwake", alisema Kassim Mganga.

Kassim Mganga si msanii wa kwanza kutoa siri hiyo kuwa wasanii wanaigiza maisha na kuwadanganya mashabiki, kwani hata msaniii Nikki wa Pili alishawahi kuzungumzia suala hilo, hata kutoa wimbo wa 'role model', ambao unawakanya vijana wanaoiga maisha ya wasanii.