Waendesha Bodaboda Nao Wautosa ‘UKUTA’

Dar es Salaam
VIONGOZI Umoja wa Vyama vya Waendesha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam leo wamewapiga marufuku wanachama wao kushiriki masuala oyote ya kisiasa hapa nchini ikiwemo maandamano hususani yaliyopewa jina la Oparesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA) yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kupangwa kufanyika kesho Alhamisi, Septemba 1, 2016.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam leo Jumatano na Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda Wilaya ya Kinondoni, Bw. Leonard Mdede wakati akizungumza na wanahabari na kusema kuwa, dereva bodaboda yeyote atakayekamatwa akijihusisha na masuala ya kisiasa au maandamano ya kisiasa atachukuliwa hatua kali za kisheria na uongozi wa chama hicho.

Aidha Bw. Leonard Mdede amewataka waendesha bodaboda wote wasibebe abiria yeyote atakakuwa amevalia sare ya chama chochote cha siasa cha hapa nchini na kusema kwa kufanya hivyo atakuwa amevunja sheria waliyojiwekea hivyo atawajibishwa ipasavyo kwa mujibu wa katiba na sheria zao.