Watendaji 4 wa vijiji na kata ya Kwimba wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za ubadhilifu.

Maafisa watendaji wanne wa vijiji na kata katika wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wanashikiliwa na askari polisi wa kituo kikuu cha Ngudu wilayani humo kwa amri ya mkuu wa wilaya hiyo Mhandisi Mtemi Msafiri kwa tuhuma za kuikosesha mapato serikali, baada ya kudaiwa kushirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kutorosha mazao nyakati za usiku.

Mkuu wa wilaya ya Kwimba, Mhandisi Mtemi Msafiri amewataja maofisa watendaji wa kata walioswekwa mahabusu ya kituo kikuu cha polisi Ngudu kuwa ni Ndalawa Masala ambaye ni afisa mtendaji wa kata ya Ngudu na John Nyanda ambaye ni afisa mtendaji wa kijiji cha Shigumlo. Aidha afisa mtendaji wa kijiji cha Hungumalwa Kazimir Maige pamoja na afisa mtendaji wa kata ya Hungumalwa Makoye Nduta wameachiliwa kwa dhamana.

Katika kituo kikuu cha polisi Ngudu, ITV ilishuhudia tani 30 za dengu zilizokamatwa na mkuu wa wilaya ya Kwimba, baada ya afisa mtendaji wa kata ya Ngudu Ndalawa Masala kudaiwa kutoa stakabadhi ya shilingi laki nane badala ya shilingi milioni moja na laki mbili, iliyokuwa imelipwa kama ushuru na mfanyabiashara John Masanja.

Diwani wa kata ya Hungumalwa Shija Malando pamoja na diwani wa kata ya Ngudu mjini Malifedha Mfuruki wamedai kuwa utoroshaji wa mazao nyakati za usiku unachangia kuipotezea mapato halmashauri ya wilaya Kwimba na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya watendaji wazembe.