FA Kuzitupa Fulana 4000 za Big Sam

Chama cha soka cha Uingereza, FA, kimelazimika ‘kuzitupa’ fulana (T-shirts) 4,000 zilizokuwa zitolewe kwa mashabiki katika mechi ya Uingereza dhidi ya Malta – kwa sababu zilikuwa na ujumbe wa maandishi kutoka kwa Sam Allardyce (Big Sam) kwa mbele.

Allardyce, 61, alikuwa anajiandaa kuiongoza Uingereza katika mechi yake ya kwanza katika uwanja wa Wembley akiwa kama kocha wa Simba Watatu (Three Lions) lakini alipoteza kazi yake baada ya siku 67 tu kutokana na habari za kujihusisha na kitendo cha kutaka kushiriki katika mchakato wa kupindisha sheria za umiliki wa wachezaji.

FA walitaka kuinogesha mechi yake ya kwanza katika uwanja wa nyumbani, kwenye mchezo wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia, Oktoba 8 kwa fulana ambazo ziliandikwa ujumbe unaosomeka hivi: ‘Safari inaanza na sisi sote kuungana pamoja’ (The journey starts with us all pulling together)

Ujumbe huu ulitokana na maneno aliyoyasema Allardyce katika siku aliyotangazwa kuwa mrithi wa Roy Hodgson.

Usitishwaji huo matumizi ya fulana hizo umeigharimu FA Paundi 25,000 sawa na milioni 70 shilingi za Kitanzania.