Gesi, mafuta vyagundulika Morogoro

KAMPUNI ya Swala energy ya hapa nchini, imefanikiwa kuona viashiria vya gesi na mafuta ghafi katika wilaya ya Kilosa, kijiji cha Kilombero mkoani Morogoro

Hayo yamesemwa na Mhandisi Felix Nanguka katika semina ya waandishi wa habari Morogoro, iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Injinia Nanguka amesema utafiti huo ulianza mwaka 2012 ambapo walitarajia kuanza uchimbaji mwishoni mwa mwaka huu.

“Kampuni ya Swala energy ilitegemea kuanza uchimbaji mwaka huu, lakini kutokana na miundombinu kutokamilika, wataanza mwaka 2017 katika kipindi cha kiangazi’’ amesema.

Aidha alisema kampuni hiyo itachimba kisima kimoja cha utafiti kijulikanacho kama kito-1 katika kitalu hicho cha Kilosa-Kilombero, ambapo wanatarajia kupata mafuta ghafi kiasi kinachokadiriwa kufika mapipa milioni 180 katika kitalu hicho.

Francis Lupokela, afisa uhusiano wa TPDC amesema, eneo lililogundulika kuwepo kwa mafuta na gesi kutakuwana shughuli nyingi za uwekezaji.

“Kupitia shughuli hizo za uwekezaji, wananchi wa maeneo hayo, watapata fursa ya kunufaika na uwekezaji huo ikiwa ni pamoja na kupata ajira kama vibarua watakaokuwa katika mradi huo,” amesema.

Pia amedokeza kuwa, mradi huo utasaidia viwanda vya jirani kupata nishati hiyo kwa gharama nafuu, ukilinganisha na gharama za nishati wanazopata kwa sasa, kwani  matumizi ya gesi asilia  hupunguza gharama kuliko nishati zingine.

“Manufaa mengine wananchi watayapata kama inavyoainishwa kupitia Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, inayobainisha wajibu wa shirika au kampuni inayowekeza eneo husika katika kusaidia masuala ya maendeleo ya kijamii katika eneo hilo,” amesisitiza.