Maadhimisho ya siku ya wazee duniani ni moja kati ya jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) katika kutambua na kuhamasisha jamii kuweza kulinda na kutetea haki za wazee duniani kote. Umoja wa Mataifa umetenga siku hii kwa lengo la kutafakari hali ya maisha ya wazee na changamoto zinazowakabili wazee; na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuboresha maisha yao na kuwafanya waishi maisha ya heshima, hadhi, na kuthaminiwa utu wao.
Kila mwaka, Maadhimisho haya huwa yanabeba Kauli Mbiu yenye ujumbe mahsusi. Kwa mwaka 2016 Kaulimbiu inasema “Zuia Unyanyasaji dhidi ya Wazee”. Kaulimbiu hii inahimiza Serikali, jamii, na wadau wengine kutafakari na kuweka mikakati ya kukabiliana na vitendo vya ukatili, mauaji, ubaguzi na dhuluma dhidi ya wazee; vitendo ambayo ni kinyume dhidi ya haki za binadamu.
Maadhimisho haya kwa mwaka 2016 yanafanyika Kitaifa katika wilaya ya Mbalali, mkoani Mbeya. Kilele cha maadhimisho haya kitajumuisha shughuli mbalimbali ikiwemo huduma ya upimaji wa hiari wa afya na ushauri kwa wazee, michezo na maonesho ya bidhaa na kazi mbalimbali zinazofanywa na wazee.
Katika kipindi hiki cha Maadhimisho hatuna budi kuenzi na kudumisha mila na desturi nzuri za kuwaenzi wazee kwa kutambua kuwa wazee ndiyo chanzo cha urithi wa historia ya nchi, washauri wa familia na jamii, watu wenye hekima, na walezi katika jamii. Hivyo jamii inaowajibu wa kuwaondolea vikwazo wazee katika kupata huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua pale ambapo mzee ananyanyashwa au kutendewa isivyostahili.
Erasto T. Ching’oro
Msemaji wa Wizara
30/9/2016.