Mashabiki Simba Vs Yanga watakiwa kutii sheria

Jeshi la Polisi limewataka mashabiki wa soka nchini kuzingatia sheria bila ya shuruti katika mpambano wa watani wa Jadi Simba dhidi ya Yanga utakaopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro amesema, wamejipanga kuhakikisha amani inakuwepo kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa mchezo na kuhakikisha kila mwananchi anaondoka akiwa salama.

Sirro amesema, wamejipanga pia kuzuia waharibifu wa miundombinu ya uwanja kuanzia mwanzo wa mchezo mpaka mwisho huku akiwataka mashabiki kuzingatia utaratibu uliotolewa juu ya upatikanaji na matumizi ya tiketi za kielektroniki zitakazoanza kutumika katika mchezo huo.

Sirro amesema, wanashirikiana na Shirikisho la Soka nchini ili kuhakikisha mashabiki wanaingia uwanjani kihalali kwa kutumia tiketi zilizohalalishwa.