Rais Magufuli ajivunia uimara wa Jeshi la Wananchi

Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, amefunga maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kushuhudia zoezi la medani liitwalo ''Amphibious Landing'' lililofanyika Bagamoyo Mkoani Pwani.

Zoezi hilo lililochukua muda wa wiki mbili, limeshirikisha kamandi zote tano za JWTZ ambazo ni Nyika, Majini, Anga, Kamandi ya Makao Makuu na Jeshi la Kujenga taifa limefanyika katika ufukwe wa bahari ya Hindi na limetekelezwa kwa mfano wa mapambano ya kivita yaliyohusisha kutua nchi kavu kutoka majini na kukomboa eneo lililotekwa.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Rais na Amiri jeshi Mkuu Dkt.John Pombe Magufuli amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange pamoja na Makamanda na Wapiganaji wote wa JWTZ walioshiriki katika zoezi hilo ambalo limefanywa kwa umakini, uhakika na weledi wa hali ya juu.

''Kweli nimefurahi na nimeamini tuna wapiganaji wa kutosha katika maeneo yote, hii mikakati na mipango iliyotumika inaonesha tuna jeshi imara na linaloaminika'' amesema Dkt. Magufuli.

Rais na Amiri Jeshi Mkuu amewahakikishia Makamanda na Wapiganaji wote wa JWTZ kuwa Serikali yake itahakikisha inaendeleza na kuongeza zaidi juhudi zilizofanywa na Marais waliopita kwa kuimarisha na kuwa na jeshi la kisasa linalotumia vifaa na teknoljia ya kisasa na pia itahakikisha maslai ya askari yanaboreshwa.

Aidha, Dkt. Magufuli ametaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuimarishwa zaidi na kujielekeza katika uzalishaji mali ikiwemo uwekezaji katika viwanda

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye pamoja na kuipongeza JWTZ amesema miaka 52 tangu kuanzishwa kwa Jeshi hilo Watanzania wanashuhudia jeshi lao likiwa imara na makini zaidi kwa ajili ya kulinda nchi.

Nae Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange amemshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake na nia yake ya kuliimarisha Jeshi na kuboresha maslai ya Makamanda na Wapiganaji na ameongeza kuwa anajivunia kuwa kiongozi wa Jeshi hilo.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Viongozi wengine wakiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar Abdulhamid Yahaya Mzee.

Rais na Amiri Jeshi Mkuu amemuagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange kuwapa ajira za JWTZ askari mgambo wote walioshiriki zoezi la Amphibious Landing.