Serikali kutoa mkopo kiwanda cha nyanya

CHARLES Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, amesema serikali itatoa mkopo kwa Mwekezaji atakayejitokeza kujenga  kiwanda cha kuchakata na kusindika nyanya mkoani Morogoro

Mwijage ameyasema hayo katika kongamano la uwekezaji la Mkoa wa Morogoro, linalofanyika mjini hapa na kuwahusisha wafanyabiashara, wawekezaji na mabalozi kwa lenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji.

“Tayari Serikali imeshazungumza na taasisi za kifedha pamoja na zipo tayari kutoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho mara moja.

Taasisi hizo za fedha ni pamoja na Benki ya NBC, CRDB na mfuko wa pensheni wa LAPF,” amesema.

Kwa mujibu wa Waziri Mwijage, uamuzi ya kuzungumza na taasisi hizo unatokana na zao la nyanya kuzalishwa kwa wingi katika mkoa wa Morogoro huku wakulima wakikosa masoko na jambo linalosababisha nyanya hizo kuharibika.

“Nia ya Serikali ni kukuza uchumi ili angalau kufikia uchumi wa kati. Tunaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ili kufikia lengo,” amesema Mwijage.

Kwa upande wake Dk. Stephen Kebwe, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, amesema kuwa kongamano hilo lina lengo kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika mkoa huo ili kuwashawishi na kuwavutia wawekezaji wenye nia ya kuwekeza hapa nchini.