Wanafunzi 141 Mwanza, wapata ujauzito mwaka huu

Jumla ya wanafunzi 141 wa shule za msingi na sekondari mkoa wa Mwanza wamepata ujauzito na wengine 143 wametoroshwa na wanaume katika kipindi cha Januari hadi Julai mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na afisa kitengo cha polisi jamii mkoa wa Mwanza, Mwita Robert Mwita, amesema matukio 149 ya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana yametokea mkoani Mwaza yametokea ikilinganishwa na matukio 447 yaliyotokea mwaka jana.

Bw. Mwita ametoa takwimu hizo katika mafunzo kwa wadau wanaojihusisha na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili ambapo walikuwa wanajengea uwezo wa kufanikisha kampeni ya 'Tunaweza' inayolenga kuondoa aina zote za ukatili mkoani humo.

Kampeni hiyo inaendeshwa na shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na harakati za kutetea haki za wanawake na wasichana mkoani humo la Kivulini baada ya kuonekana vitendo hivyo vinazidi kuongezeka.

Mkurugenzi wa shirika hilo Bw. Yasin Ally amesema kuwa kuna baadhi ya wazazi wanachangia ongezeko la matukio ya mimba za utotoni baada ya kufikia makubaliano na watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi, hivyo shirika hilo kupata ugumu katika harakati za kukomesha tatizo hilo.