Hatuwezi kuingilia sakata la Lema na Gambo Arusha

Tume ya Haki za BInadamu na Utawala Bora imesema kuwa licha ya kuwa na wajibu wa kusimamia masuala ya utawala bora, haiwezi kuingilia kati mgogoro uliopo kati ya viongozi wa kuchaguliwa mkoani Arusha na viongozi wa kuteuliwa na Rais.

Kamishna wa tume hiyo, Dkt. Kevin Mandopi amesema kuwa suala la migogoro inayohusisha viongozi, linashughulikiwa na Sekretariet ya Maadili ya Viongozi wa Umma, na siyo tume hiyo moja kwa moja.

Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku chache baada ya kutokea kwa mgongano ulioibua mabishano ya hadharani kati ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, kuhusu upatikanaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali.