JPM atakiwa kuieleza ukweli Morocco kuhusu Sahara

 Kamati ya mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi TASSC imemtaka Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuendeleza msimamo wa Tanzania kuHusiana na mgogoro wa Morocco na Sahara Magaribi.

Tamko hilo limekuja siku moja kabla ya ujio wa Mfalme wa Morocco, Mohamed VI ambaye anatarajiwa kufanya ziara nchini Tanzania kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 25 mwezi huu na kupokelewa na mwenyeji wake Rais Magufuli ambapo mikataba 16 ya kimaendeleo itasainiwa.
Akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari hii leo jijini Dar es salaam Katibu wa Kamati ya TASSC Jaspar Sabuni amesema Tanzania ikiyumba kuhusiana na suala hilo ni kwenda kinyume na muasisi wa Taifa hili Hayati Julius Nyerere ambaye alipigania mataifa mengine kupata uhuru wao hasa wanyonge.

“Tunaamini Rais Magufuli hayumbishwi, amwambie Mfalme Mohamed wa VI wa Morocco kuwa Sahara Magharibi ni lazima iachiwe huru sambamba na wafungwa wote wa kisiasa wanaogombania uhuru wa Sahara Magharibi” amesema.

 Naye Mratibu wa Mawasiliano kwa Umma wa kamati hiyo bwana Noel C. Shao, amesema Afrika haiwezi kuwa huru mpaka pale nchi zote za eneo hilo zitakapokuwa huru na kwamba kitendo cha Morocco kuendelea kuitawala Sahara Magharibi kimabavu hakivumiliki

Sahara Magharibi imetawaliwa kimabavu na Morocco kwa miaka 40 sasa licha ya jitihada za umoja wa Afrika na wito wa Umoja wa Mataifa wa kuitaka Moroco kuipatia uhuru Sahara Magharibi