Kiboko Mnyama Mwenye Jasho Jekundu

KIBOKO ni miongoni mwa mamalia mkubwa wa familia ya Hippopotamidae. Anapatikana zaidi katika bara la Afrika na anasifika kwa kinywa na meno yake makubwa. Pua, macho na masikio ya kiboko yapo juu ya fuvu la kichwa hali inayomuwezesha kuzamisha sehemu kubwa ya mwili wake kwenye maji au matope na kupata ubaridi kujizuia na mwanga mkali wa jua.

Kiboko hawezi kukaa nchi kavu nyakati za mchana kwa sababu ngozi yake inaathiriwa na mwaka wa jua. Wakiwa majini ngozi zao hutoa majimaji mekendu kwa ajili ya kuzuia kuungua na jua. Ingawa majimaji hayo sio jasho wala damu ni maarufu kwa jina la ‘jasho jekundu.’

Wataalamu wanasema majimaji hayo hutoka kwenye ngozi ya kiboko bila rangi yoyote lakini baada ya muda mfupi huwa mekundu na baada ya saa chache huwa ya kijivu. Wataalamu wanasema maji hayo hubadilika rangi kwa sababu yana kemikali aina mbili zinazofahamika ‘hipposudoric acid’ na ‘norhipposudiric acid’ kwa jina la kitaalamu.

Kemikali hizi zina kazi muhimu katika mwili wa kiboko kwa kuwa huzuia ukuaji wa bakteria wanaosababisha magonjwa na kuzuia ngozi ya kiboko dhidi ya athari zinazotokana na mionzi ya jua. Viboko huhesabiwa kama wanyama wakubwa nchi kavu lakini tofauti na wanyama wengine wakubwa , viboko huishi kwenye maji baridi ya mito na maziwa. Unene wao unawaruhusu kuzama na kuogelea kwenye kina cha chini kabisa cha mto au ziwa.

Kiboko anafananishwa na nguruwe kwa sababu ana kwato na mwili wake una mafuta mengi mithili ya nguruwe. Wapo watu wanaomuita nguruwe maji. Hata hivyo mwili wa kiboko hauna manyoya, ana miguu mifupi na umbo kubwa. Kimo cha mabegani kinafikia mita 1.5 na ana urefu wa mita mita 4.5. Ingawa kiboko ni mnene na ana miguu mifupi ana uwezo wa kukimbia mwendo wa kilomita 48 kwa saa moja.

Hata hivyo taarifa za mwendo kasi wa kiboko zinatofautiana kutokana na maeneo kwa kuwa baadhi ya wanasayansi wanasema anakimbia kwa kilomita 29 kwa saa moja hivyo ana mbio za kasi kuliko binadamu. Kiboko ni mnyama mwenye uwezo wa kuishi majini na nchi kavu. Huishi kwenye maji baridi katika mito na maziwa lakini ana uwezo wa kutembea kwenye nchi kavu mbali na maji.

Kiboko anaishi kwa kula majani na inasemekana kuwa ni mnyama mkorofi na huenda anashikilia nafasi ya kwanza miongoni mwa wanyama wasiopatana na binadamu. Wataalamu wanasema watoto wa simba, chui, fisi, tembo, au nyati akikulia katika makazi ya binadamu wanaweza kuishi bila kuleta madhara makubwa lakini kiboko hana huruma anapokutana na binadamu.

Hata hivyo sio rahisi kumpata mtoto wa kiboko na kumuweka katika makazi ya binadamu kwa kuwa kiboko huzalia majini na ana utaratibu wa kulea mtoto kwa miezi minane hadi mwaka mmoja ndipo anaacha kunyonya. Kiboko anashindana na kifaru mweupe katika kugombea nafasi ya pili ya mnyama mzito kwenye nchi kavu baada ya tembo ambaye anashikilia nafasi ya kwanza ya mnyama mkubwa wa nchi kavu ana uzito wa kilogramu 3,000 hadi 7,000 sawa na tani tatu hadi tani saba.

Taarifa za hivi karibuni zinasema kiboko anashikilia nafasi ya tatu ya mnyama wa nchi kavu akiwa na uzito kati ya kilogramu 1,500 na 3,500 sawa wa tani moja na nusu hadi tani nne wakati faru mweupe ana uzito wa tani 1,500 hadi 4,000 sawa na tani moja na nusu hadi tani nne. Hata hivyo baadhi ya wanasayansi wanasema huenda kiboko ana uzito zaidi lakini hajaweza kuthibitishwa kwa sababu umbo lao kubwa inakuwa vigumu kumpima uzito wao wakiwa mwituni wakati wa kula majani.

Sio rahisi kuwawekea kizuizi wala kuwakaribia wakiwa majini kwa kuwa ni hatari. Makadirio mengi ya uzito yanatokana na operesheni za kuwapunguza zilizofanyika mnamo 1960. Wastani wa uzito kwa kiboko dume ni kati ya kilogramu 1500 hadi 1800. Viboko jike ni wadogo kidogo wakiwa na wastani wa uzito wa kilogramu 1300 hadi 1500. Viboko wakubwa dume wanaweza kuwa wakubwa sana mpaka kufikia kilogramu 4,500 jambo linaloashiria kuwa wanaweza kuwa na uzito mkubwa kuliko faru mweupe.

Viboko dume huendelea kukua muda wote wa maisha yao, huku majike hufikia uzito wa juu wakifikia umri wa miaka 25. Kiboko huishi majini na nchi kavu, hasa kwenye maziwa na mito ambako viboko dume humiliki eneo kubwa linalotosha kuishi ambapo kundi la viboko jike watano hadi 30 huishi pamoja wakiwa na watoto wao. Wakati wa mchana kiboko hubaki wametulia kwa kukaa ndani ya maji au matope huku wakiweka vinywa vyao juu ili kuvuta hewa. Kiboko hujamiiana na kuzaa wakiwa ndani ya maji.

Kwa kuwa mtoto wa kiboko huzaliwa kwenye kina kifupi cha maji huogelea na kuja juu ya maji ili kuvuta hewa. Kwa kawaida kiboko huzaa mtoto ila mara chache kutokea mapacha. Mtoto wa kiboko huzaliwa akiwa na uzito wa kilogramu 45 hadi 70 na hunyonya maziwa ya mama yake mara baada ya kuzaliwa na baada ya wiki chache kujifunza kutoka majini na kwenda kutafuta chakula.

Kiboko jike hupevuka akiwa na umri kati ya miaka minne na mitano ila kiboko dume hupevuka akiwa na umri wa miaka saba na nusu. Ingawa viboko hupumzika pamoja ndani ya maji, wakati wa kwenda kula nyasi hutawanyika nchi kavu na kila mmoja kula sehemu yake pasipo kuwekeana mipaka. Hata kama nyasi ziko mbali kiboko ana uwezo wa kukimbia umbali mrefu kwa muda mfupi ili kufuata nyasi.

Ingawa kiboko kufanana kimaumbile na nguruwe inadaiwa viboko wana uhusiano wa karibu na nyangumi kwa kuwa chimbuko la uhai wao ni moja. Nyangumi na wanyama wengine ambao kitaalamu wanaitwa “sesataseani”, porpoises walikuwa jamii moja ila waligawanyika zaidi ya miaka milioni 55 iliyopita. Mnyama wa kale asili ya nyangumi na kiboko aligawanyika kutoka jamii nyingine za wanyama wenye kwato nne mnamo miaka milioni 60 iliyopita.

Mabaki ya kale zaidi ya kiboko ni ya jenasi Kenyapotamus yanayopatikana barani Afrika na yaligunduliwa miaka milioni 16 iliyopita. Kuna kadiri ya viboko 125,000 mpaka 150,000 katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara; Zambia 40,000 na Tanzania 20, 000 mpaka 30,000. Viboko bado wapo kwenye tishio la kutoweka kutokana na kutoweka kwa uoto wa asili karibu na mito na maziwa.

Ujangili uliokithiri pia unasababisha hatari ya kutoweka kwa wanyama hao adimu kwa sababu ya tamaa ya watu wachache wenye uchu wa kula nyama ya kiboko na kuuza memo yao bila kujali umuhimu wake katika elimu ya viumbe kwa ngazi ya kitaifa na kimataifa. Kiboko ana uwezo wa kuishi kati ya miaka 30 hadi 50 ikiwa hata bughudhiwa wala kujeruhiwa.

Kiboko anaitwa Donna aliyekuwa kwenye hifadhi ya wanyama nchini Marekani anashikiliwa nafasi ya kwanza ya kiboko jike aliyeishi miaka mingi zaidi kwani alikufa akiwa na umri wa miaka 57. Kiboko dume anaitwa Tanga alikufa akiwa na umri wa miaka 61 katika hifadhi ya wanyama nchini Ujerumani na kuacha historia ya kiboko dume aliyeishi muda mrefu zaidi na ni kielelezo kuwa kiboko dume huishi miaka mingi kuliko jike.