Ligi ya soka ya wanawake yaanza kutimua vumbi

Ligi ya Taifa ya Wanawake inatarajiwa kuanza kesho Jumanne Novemba 1, 2016 kwa viwanja sita kuchezwa mechi za ufunguzi.

Hafla ya uzinduzi wa ligi hiyo utafanyika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma katika mchezo ambao Baobao ya hapo itakapocheza na Victoria Queens ya Kagera.

Viongozi mbalimbali wa serikali wakiwamo mawaziri na wabunge ambao kwa sasa wako kwenye vikao mjini Dodoma kwa pamoja wanatarajiwa kuwa katika hafla hiyo ambayo pilikapilika zake zinatarajiwa kuanza saa 8.00 mchana kabla ya mchezo kuanza saa 10.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Mbali ya mchezo huo wa kundi B kati ya Baobao na Victoria, michezo mingine itakuwa ni kati ya Sisterz na Panama utakaofanyika Uwanja wa Tanganyika huko Kigoma wakati Marsh Academy ya Mwanza itacheza na Majengo Women ya Singida kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kundi A kutakuwa na michezo mitatu ambako Viva Queens ya Mtwara itacheza na Mburahati Queens ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona wakati Fair Play ya Tanga itapambana na Evergreen ya Dar Salaam katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga huku JKT Queens ikiwa ni wenyeji wa Mlandizi Queens ya Pwani kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.