Magufuli: Kenya ni mshirika wetu nambari moja Afrika

 Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema kuwa Kenya ndio mshirika nambari moja wa Tanzania katika uwekezaji na biashara barani Afrika.

Akizungumza katika ikulu ya rais jijini Nairobi mda mfupi baada ya kuwasili nchini Kenya,Rais Magufuli amesisitiza kuwa hakuna taifa jingine ambalo limewekeza nchini mwake kama Kenya.

Amesema kuwa kulingana na rekodi za uwekezaji nchini Tanzania kuna takriban kampuni 529 nchini humo kutoka Kenya ambazo zinaingiza takriban dola bilioni 1.7 kila mwaka huku takriban Watanzania 57,260 wakiwa wameajiriwa.

Rais huyo vilevile ametoa wito kwa Wakenya wanaotaka kuwekeza nchini Tanzania kuharakisha hatua hiyo.

Aidha ameongezea kuwa amekuwa akiwasiliana na rais Uhuru Kenyatta mara kwa mara na kuwakosoa wale wanaodhani kwamba uhusiano wake na rais wa Kenya una utata.

Magufuli aliwasili nchini Kenya mapema siku ya Jumanne ambapo alilakiwa na waziri wa maswala ya kigeni Amina Mohammed kabla ya kuelekea katika ikulu ya State house ambapo alifanya mazungumzo na mwenyeji wake rais Uhuru Kenyatta.

 Msemaji wa Rais Kenyatta, Manoah Esipisu, Jumapili aligusia baadhi ya mambo ambayo Kenya inatarajia kutoka kwa ziara ya Rais Magufuli nchini Kenya.

Alisema: "Ziara ya Rais huyu inatupatia fursa ya kufanya upya na kukoleza uhusiano wetu katika nyanja mbalimbali. Viongozi wa nchi hizi watashauriana kuhusu masuala mbalimbali ya pamoja katika ngazi ya taifa kwa taifa na kanda. Wataangazia sana masuala ambayo tayari kumekuwa na mazungumzo, na tunatarajia matokeo ya mazungumzo hayo kutangazwa.

"Masuala kadha yatajadiliwa, ikiwemo ada ya vibali vya kufanyia kazi ambayo raia wa Kenya hutozwa, pamoja na karo ya juu ambayo Wakenya hutozwa vyuo vikuu (Tanzania). Mashauriano kuhusu kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hizi mbili pia yatafanyika. Kadhalika, na muhimu sana katika mazungumzo hayo ni shughuli za magari ya kusafirisha watalii yanayovuka mipaka.

"Muhimu katika mashauriano haya itakuwa pia kufufuliwa kwa Tume ya Ushirikiano wa Pamoja na Tanzania (JCC) ambayo ni jukwaa ambalo linaweza kutumiwa kutangaza biashara na uwekezaji baina ya nchi zote mbili.

"Rais Kenyatta pia atazungumza na Rais Magufuli kumhusu Bi Amina Mohammed (waziri wa mambo ya nje wa Kenya) anayewania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.