Mbegu ya Pamba aina ya UK 91 haitazalishwa kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017.

Mbegu ya pamba yenye manyoya ya uk 91 haitazalishwa katika msimu wa kilimo cha pamba wa mwaka 2016/2017,unaotarajia kuanza mwezi Novemba mwaka huu,baada ya mbegu hiyo kukosa ubora na kupitwa na wakati.

Mkurugenzi wa huduma za usimamizi kutoka Bodi ya pamba nchini James Shinde amesema mbegu ya UK 91 ya manyoya imedumu muda mrefu sokoni na kupoteza ubora wake na kuongeza kwamba mpaka sasa kuna mbegu 2,090 za UKM 08 kwa ajili ya kusambazwa katika maeneo ya mkoa wa Singida na Tabora katika wilaya ya Igunga kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora za pamba katika msimu huu wa kilimo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la kilimo na mifugo Tanzania,Janeth Bitegeko,amesema kilimo hicho kimeendelea kushuka na kusababisha umaskini kwa wakulima kutokana na kukabiliwa na tatizo la mbegu hafifu.

Prof.Reuben Kadigi,Mhadhiri kutoka shule ya uchumi,kilimo na stadi za biashara,ya Chuo Kikuu cha kilimo Sokoine Morogoro (SUA ) anasema sekta ya pamba bado inakabiliwa na changamoto nyingi zitakazosababisha wakulima kujiondoa kuendelea na zao hilo,zikiwemo za ukosekanaji wa pembejeo.

Zao la pamba hulimwa na wakulima wanaokadiriwa kuwa laki tano katika mikoa 15 na wilaya 46 za Tanzania bara,mikoa ya Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Simiyu,Shinyanga,Mara, Geita,Kigoma,Kagera,Tabora,Singida na Mwanza inazalisha takribani asilimia 99 ya pamba yote nchini.