Nape, Zitto wavaana muswada wa habari-1

Baada ya kupambana na mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, vita kuhusu Muswada wa Huduma za Habari umehamia nje ya chombo hicho, safari hii Zitto Kabwe akipambana na Wazari ya Habari, Nape Nnauye.

Vita baina ya wawili hao inafanyika kwenye mitandao ya kijamii ambako Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, ametoa maoni yake kuhusu muswada huo na baadaye Nape kumjibu kabla ya Zitto kumjibu tena.

Zitto, ambaye aling’ara alipoingia bungeni akiwa kijana mdogo na kuchachafya chombo hicho kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja, alipambana vikali na Peter Serukamba wakati muswada huo uliposomwa kwenye kamati hiyo mapema wiki hii.

Hoja ya Zitto ilianzia katika kutaka kujua ni kiasi gani wadau wa habari wameshirikishwa katika kuupitia muswada huo, huku Serukamba, ambaye ni mwenyekiti wa kamati akitoa ufafanuzi.

Vita ya Zitto na Nape

Zitto, ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, alitoa waraka kwenye mitandao ya jamii akiuponda muswada huo kwa kuuita kuwa ni“hatari”.