RC Gambo apokea msaada wa bati 500 na mifuko ya sarufi 500

Nteghenjwa Hosseah - Arusha
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amepokea msaada wa bati 500 pamoja na mifuko ya saruji 500 kwa ajili ya kuwezesha huduma mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati pamoja na shule za msingi na sekondari za Mkoa wa Arusha.

Mara baada ya kukabidhi wa msaada huo nje ya jengo la Ofisi ya Mkuu huyo, Gambo alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Dararro mifuko 100 ya saruji na mabati 100  kwa ajili ya ujenzi kituo cha afya kinachojengwa eneo la kwa mama mbauda kata ya Muriet Jijini Arusha.

Alisema msaada huo utawezesha kila wilaya kunufaika nao kwani kila wilaya za mkoa wa Arusha kuna changamoto za uhaba wa vyumba vya madarasa pamoja na mahitaji ya majengo ya zahanati ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Alimshukuru Meneja Mradi wa Kampuni ya ujenzi ya Hanil - Jiangsu Joint Venture Ltd, inayojenga barabara ya Sakina  - Tengeru Km 14.1 na barabara ya Mchepuko Km 42.4 , Xie Jianbao ambao wametoa msaada huo kama sehemu ya kurudhisha kwa jamii ya watanzania ili kukuza mahusiano na kujali jamii na Taifa ambalo limewapa kazi kubwa ya ujenzi wa barabar hiyo itakayogharimu takribani Bil. 139.

"Naishukuru kampuni hii kwa kutoa msaada huo kwa ajili ya kuleta maendeleo na naahidi tutautumia ipasavyo katika kuleta maendeleo na kila wilaya nitakayofanya ziara msaada huo nitaupeleka ili ya kupunguza changamoto mbalimbali kwa jamii ".

Naye Meneja Mradi wa kampuni hiyo, Bw. Xie alisema kampuni yao imeona umuhimu wa kuchangia jamii kwani wao ni wajenzi wa barabara na wanastahili kurejesha faida kwa jamii inayowazunguka.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Gabriel Daqarro alimshukuru Gambo kwa msaada huo na kusisitiza kuwa mifuko hiyo 100 ya saruji pamoja na bati 100 zitasaidia ujenzi wa kituo cha afya kinachojengwa Kata ya Muriet Jijini Arusha.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia alishukuru kwa msaada huo utakaosaidia ujenzi wa kituo cha afya kujengwa na kukamilika ndani ya miezi miwili na kuahidi kwamba atasimamia ipasavyo ili kuhakikisha Kituo kinajengwa katia ubora unaostahili.

Katika  makabidhiano hayo yaliyohudhuriwa na  wabunge wa Viti maalum wanawake Mkoa wa Arusha, Catherine Magige na Aminah Mollel walitoa rai kwa nyakati tofauti kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kumuunga mkono Mhe. Gambo pamoja na Serikali ili kuwezesha maendeleo kusonga mbele.