Sababu ya chombo cha Ulaya kutoweka Mars

Shirika la Anga za Juu la Ulaya (ESA) ambalo lilituma chombo cha anga za juu kwa jina Schiaparelli limeeleza sababu ambazo huenda zilichangia chombo hicho kutoweka Jumatano.

Chombo hicho kilitarajiwa kutua kwenye sayari hiyo lakini mawasiliano yakakatika ghafla na kuzua wasiwasi.

Maafisa sasa wanasema parachuti (mwavuli) ambayo ilifaa kutumiwa na chombo hicho kutua salama ilitengana na chombo hicho mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Aidha, roketi ambazo zilifaa kusaidia chombo hicho kusimama angani muda mfupi kabla ya kufika kwenye 'ardhi' ya Mars pia ziliwaka kwa muda mfupi sana kuliko ilivyofaa.

Uamuzi huo umetokana na data ambayo roboti iliyo kwenye chombo hicho cha Schiaparelli iliweza kutuma kwa chombo mama kwa jina Trace Gas Orbiter (TGO) ambacho kilibaki kikiizunguka sayari hiyo.

Maafisa wa ESA wanasema kufikia sasa bado hawajakata tamaa kabisa kuhusu hatima ya chombo hicho, ingawa hawana matumaini sana.

Kuna uwezekano kwamba chombo hicho kilifikia sayari hiyo kikienda kwa kasi isiyofaa na hivyo kikaharibika.

Wataalamu mjini Darmstadt, Ujerumani wanaendelea kutathmni data kutoka kwa TGO, na huenda wakajaribu kuona iwapo watafanikiwa kuwasiliana na roboti ya Schiaparelli, wakiomba kwamba chombo hicho kiwe salama kwenye sayari hiyo.

Walifanikiwa kupata data ya ukubwa wa megabaiti 600 kutoka kwa chombo hicho kilichogharimu dola 251 milioni kabla ya mawasiliano kukatika.

Wanasema hali kwamba kuna data nyingi ambayo chombo hicho cha Schiaparelli kiliweza kutuma kwa TGO inaashiria kwamba chombo hicho kilikuwa sawa kilipokuwa kinaingia katika anga ya Mars.

Kifaa cha kukinga dhidi ya joto kali kinaonekana kilifanya kazi vyema, na parachuti ilifunga ilivyotarajiwa na kuanza kupunguza kasi ya chombo hicho.

Lakini wakati wa kutengana na chombo hicho, mambo yanaonekana kwenda kombo.
Roketi ambazo zilifaa kufunguka mara punde baadaye, wanasema, inaonekana ziliwaka kwa sekunde tatu au nne pekee. Zilitarajiwa kuwaka kwa sekunde 30.

Chombo hicho cha Schiaparelli kiliendeleza mawasiliano kwa sekunde 19 baada ya hayo kutokea, lakini sekunde 50 kabla ya wakati ambao kilitarajiwa kutua mawasiliano yakakatika.

Wataalamu hao pia watajaribu kutumia satelaiti ya Marekani ambao inaizunguka Mars kupiga picha eneo ambalo chombo hicho kilitarajiwa kutua kuona iwapo kitaonekana. Hata hivyo, matumaini ya chombo hicho kuonekana ni finyu kwani ni kidogo mno.

Wanasayansi wengi wanaamini kwamba chombo hicho kiliharibika baada ya kufika kwenye sayari hiyo kikiwa na kasi ya juu zaidi.

Ikithibitishwa kwamba chombo hicho kimepotea, itakuwa pigo kubwa kwa ESA.
Chombo hicho cha Schiaparelli kilikuwa kimesafiri kwa miezi saba umbali wa kilomita milioni 496 kikiwa kimebebwa na TGO hadi umbali wa kilomita milioni moja kutoka Mars ambapo kilitengana na kufunga safari kivyake kuelekea kwenye sayari hiyo Jumapili.

Shirika hilo lilipoteza chombo kingine kwa jina Beagle-2 ambacho kilifaa kutua kwenye safyari hiyo 2003.

Lakini maafisa wake wanasisitiza kwamba hakuna haja ya kuwa na wasiwasi sana kwamba chombo hicho kilikuwa tu cha kufanyia majaribio teknolojia na kutoa ufafanuzi zaidi kwa wataalamu.

Mradi kamili wa kutuma chombo cha kutua Mars unalenga mwaka 2021, ambacho watatuma chombo chenye magurudumu sita.