Yanga yarudi Shamba la Bibi, Simba bado

Dar es Salaam. Licha ya Yanga kuomba kutumia Uwanja wa Amaan Zanzibar kwa mechi za Ligi Kuu Bara, Bodi ya Ligi (TPL-Board), imeirudisha kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambako itaanza kuutumia kwenye mchezo wao wa Jumatano dhidi ya Mtibwa Sugar.

Wiki iliyopita, Yanga iliiandikia barua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuomba kutumia Amaan kama uwanja wake wa nyumbani baada ya Waziri wa Michezo, Nape Nnauye kuipiga marufuku timu hiyo na watani zao, Simba kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hatua ya Serikali ilikuja siku moja baada ya mchezo wa Simba na Yanga ambao mashabiki wa timu hizo walivunja mageti mawili ya Uwanja wa Taifa huku wale wa Simba waking’oa viti zaidi ya 1,700.

Baada ya Serikali kutoa zuio hilo, timu hizo zilitakiwa kuipelekea Bodi ya Ligi barua ya kuonyesha viwanja zitakavyotumia kabla ya Jumamosi iliyopita ambako Yanga iliomba kutumia Uwanja wa Amaan, Zanzibar na Simba kuomba huruma ya Serikali irejee Uwanja wa Taifa.

Ofisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura aliliambia gazeti hili jana kwamba Ligi Kuu ya Bara haiwezi kwenda kuchezewa Zanzibar.

“Yanga itacheza Uwanja wa Uhuru, kanuni hazisemi Ligi Kuu ya Bara itachezewa Zanzibar, hicho ni kitu ambacho hakiwezekani, hivyo Yanga itacheza Uwanja wa Uhuru,” alisema Wambura.

Upande wa Simba kuomba kurejea tena Taifa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel alisema wanasubiri barua yao iwafikie ofisini ndipo watatoa msimamo. “Kama wameandika barua, haijatufikia bado, tunaisubiri ifike tuone kilichoandikwa ndani ni kitu gani ndipo tutazungumza,” alisema.
Mpya zaidi Nzee zaidi