Yanga yatoa kipigo kikali kilichoacha rekodi VPL 2016-17

Story kubwa katika anga la michezo hapa Bongo ni namna ambavyo mchakato wa mabadiliko ya klabu ya Yanga unavyozidi kuchua sura mpya kila kukicha, lakini ukiweka hilo kando October 22 Yanga imetoa dozi ya maana kwa Kagera Sugar kwa kuichakaza bao 6-2 katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara.

Kagera Sugar ikiwa kwenye uwanja waje wa nyumbani Kaitaba, imeshindwa kuzuia mvua ya magoli kutoka kwa watoto wa Jangwani na kujikuta wakilazimishwa kuwa timu ya kwanza kuchezea kichapo kikubwa msimu huu huku Yanga ikiwa timu ya kwanza kufunga magoli mengi kwenye mechi moja hadi sasa tangu kuanza kwa msimu.

Kagera Sugar ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza kupitia kwa Mbaraka Yusuf katika dakika ya tatu kipindi cha kwanza akiachia shuti kali lililombabatiza Vicent Andrew na kutinga wavuni lakini Donald Ngoma akaisawazishia Yanga dakika mbili baadaye kwa kuunganisha pasi kutoka kwa Simon Msuva.

Simon Msuva akafunga bao la pili baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na golikiwa wa Kagera Sugar Hussein Sharif ‘Casillas’ wakati akiokoa shuti kali la Haruna Niyonziwa.

Yanga wakapata goli la tatu lililofungwa na Obrey Chirwa baada ya Casillas kutema mpira kwa mara ya pili na kutoa mwanya kwa Chirwa kufunga goli rahisi katika mchezo huo.

Dakika tatu baada ya timu kutoka mapumziko, Mbaraka Yusuf mfungaji wa bao la kwanza la Kagera Sugar akaifungia timu yake bao la pili na kufanya matokeo kusomeka Kagera Sugar 2-3 Yanga.