Ugonjwa hatari kuliko Ukimwi sasa tishio kwa Watanzania

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema maambukizi ya virusi vya homa ya ini (Hepatitis B) kitaifa, ni makubwa kuzidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).


Imesema kuwa katika kila watu 100 duniani, wanane wameambukizwa homa hiyo na kwamba utafiti unaonyesha uwezekano wa kupata `Hepatitis B’ ni mara 10 zaidi ya kupata maambukizi ya VVU.

Hayo yalisemwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ini na Matumbo wa MNH, Dk. John Lwegasha, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza uchunguzi na tiba bure ya ugonjwa huo katika hospitali hiyo.

Dk. Lwegasha alisema homa ya ini husababishwa na maambukizi yatokanayo na ngono zembe, kuchangia sindano, kuwekewa damu isiyopimwa na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua.