Kagera Sugar watamba kuwaangamiza Stand leo

KOCHA WA KAGERA SUGAR, MECKY MEXIME.

KOCHA wa Kagera Sugar, Mecky Mexime amesema kwamba watapambana kuhakikisha wanashinda mechi ya kwanza ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo.

Baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji Mbeya City katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili Uwanja wa Sokoine, Mbeya – leo Kagera wanarejea nyumbani Uwanja wa Kaitaba, Bukoba kuikaribisha Stand United.

Akizungumza na Nipashe jana, kocha wa Kagera, Mexime alisema kwamba anatarajia mchezo huo utakuwa mgumu, lakini watapambana waweze kushinda ili wapate pointi tatu.

“Stand United ni timu nzuri na mzunguko wa kwanza ilifanya vizuri sana, na zaidi hizi timu za Kanda ya Ziwa zinafahamika sana na kama utakumbuka msimu uliopita Kagera ilikuwa inachezea mechi zake Shinyanga, kwa hiyo utakuwa mchezo mkali, ila tutajitahidi tushinde,”alisema.

Mexime alisema anafurahi kuelekea mchezo huo wachezaji wake wote wapo fiti, hivyo ana fursa nzuri ya kuchagua wa kuwatumia ili wampe ushindi.

“Vijana wangu wote wapo vizuri na hakuna majeruhi hata mmoja,”alisema Maxime.
Mpya zaidi Nzee zaidi