Mwandishi wa ITV/Radio One Halfan Lihundi aachiwa kwa dhamana.

Mwandishi wa habari wa ITV/Radio One Arusha Halfan Lihundi  aliyekua ameshikiliwa na jeshi la polisi wilaya ya Arumeru na kuwekwa mahabusu kwa zaidi ya masaa ishirini na manne kwa kile kinachodaiwa kuwa ni agizo la mkuu wa wilaya hiyo Alexender Mnyeti ameachiliwa kwa dhamana.

Lihundi alikamatwa Disemba 21 majira ya saa 8 mchana ambapo awali alifunguliwa shitaka la kuandika habari za uchochezi, ambalo hata hivyo katika hali ya sintofahamu leo asubuhi Disemba 22, polisi katika kituo cha Usariver walikanusha kwamba hakukuwa shitaka lolote isipokua wanafuata agizo la mkuu wa wilaya la kumuweka mahabusu.

Akizungumza mara baada ya kuachiwa kwa dhamana majira ya saa 9:30 alasiri Lihundi amesema katika mahojiano na askari wa upelelezi ametuhumiwa kuandika habari nyingi zinazohusu malalamiko ya wananchi bila kile kinachoelezwa kusikiliza upande wa uongozi wa wilaya.

Mwanasheria wa mwandishi huyo kutoka tume ya haki za binadamu Edwin Silayo amesema Lihundi ameachiwa kwa dhamana ya shilingi milioni 10 na wadhamini wawili huku akitakiwa kuripoti  kituo hicho cha polisi Disemba ishirini na saba.

Tukio la kukamatwa kwa mwandishi huyu limewagusa waandishi wa habari vyombo vya habari vya  kitaifa na kimataifa wa mkoa wa Arusha ambao wameonekana kusimamisha shughuli zao na kupiga kambi katika kituo hicho kwa siku zote mbili.

Wakati waandishi wa habari wakiendelea na harakati za kufuatilia hatma ya mwenzao, wilayani Arumeru kulikua na ziara ya waziri wa ardhi, nyumba na makazi Wiliam Lukuvi ambaye alikua na kikao na viongozi na watendaji, waandishi wakafika na kutaka kuongea na mkuu wa wilaya Alexander Mnyeti na hivi ndivyo hali ilivyokua.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items