F Ngassa yupo fiti kuitumikia Mbeya City - Uongozi | Muungwana BLOG

Ngassa yupo fiti kuitumikia Mbeya City - Uongozi

Kiungo mshambuliaji wa Kimataiafa wa Tanzania Mrisho Khalfan Ngassa amejiunga rasmi na klabu ya Mbeya City inayoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania Bara, ambapo uongozi wa timu hiyo umesema kuwa yuko imara kiafya.

 
Mrisho Ngassa

Uongozi huo umelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuenea kwa taarifa kuwa Mrisho Ngassa ana majeraha ambayo yanaweza kuathiri kiwango chake dimbani, ambapo umesema kuwa madaktari wa timu wamempima na kuthibitisha kuwa yuko fiti kiafya, na hana majeraha yoyote.

"Sisi kabla mchezaji hajaanza kucheza lazima aangaliwe afya yake, kwahiyo tayari madaktari wamempima na wamethibitisha kuwa hana tatizo lolote" Imesema Mbeya City.

Mchezaji huyo ambaye amewahi kuwika na vilabu vya Yanga, Simba na Azam kabla ya kutimkia nchini Afrika Kusini na baadaye Oman, amerejea nchini na kujiunga na Mbeya City katika usajili wa dirisha dogo unaofungwa rasmi leo.

Afisa Habari wa Mbeya City Dismas Ten amesema Ngassa alitua Mbeya siku ya jana na anatarajiwa kukamilisha usajili wake leo kabla timu hiyo haijatoa taarifa ya mwisho kuhusu iliowasajili.