Jeshi la Polisi mkoa wa Morogoro limekiri kuhusika na mauaji ya watu wawili waliokufa kwa kupigwa risasi maeneo ya Kisaki Stesheni wilayani Morogoro kwa madai walifanya hivyo kukabiliana na wananchi waliokua wakizuia zoezi la kuwakamata watuhumiwa wa makosa makubwa waliopo eneo hilo.
.jpg)
Akizungumzia tukio hilo ambalo limehusisha vifo vya wananchi wawili na mmoja kujeruhiwa, kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Ulrich Matei amesema katika kijiji hicho walikwenda askari polisi katika operesheni maalumu ya kuwakamata wahalifu wa makosa makubwa ingawa hakuweka wazi makosa yao, na siku mbili baadaye walifanikiwa kuwatia watuhumiwa watatu, Ushindani Salum, Ally Ngohamweru na Musa Bakari lakini wakati ukamataji ukiendelea wananchi walifika na kuanza kuzuia kazi zoezi hilo, ingawa askari waliwasihi kuondoka bila mafanikio.
Kamanda huyo wa polisi amebainisha kuwa wananchi hao waliamua kufunga barabara kwa magogo na kurusha mawe ovyo yaliyo mjeruhi mmoja wa askari kwa madai walitaka kufahamu wanako pelekwa ndugu zao, ambapo askari hao wakaamua kupiga risasa 22 kujihami na kusababisha vifo vya watu wawili papo hapo na majeruhi mmoja, Juma Malekelea.
ITV imefika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kufahamu hali ya majeruhi Juma, baada ya taarifa za polisi kudai amelazwa hapo akiendelea na matibabu lakini uongozi wa hospitali ya mkoa ulikana kuwa na taarifa za majeruhi huyo.
Awali katika eneo la tukio, wananchi wa Kisaki Station Walidai hawakuwa na sababu ya kuzuia kazi za askari polisi kama ujumbe wao ungeanzia kwa uongozi wa kijiji na kujitambulisha, ndio sababu kubwa iliyofanya baadhi yao kuweka vizuizi kwa kuamini huenda walikuwa majambazi, na tayari miili ya waliokufa imezikwa kijijini hapo.