Wauawa baada ya kupora kituo cha mafuta

WATU watatu wanaotuhumiwa kufanya ujambazi na kupora Sh. milioni mbili katika kituo cha mafuta cha Dabalo wilayani Chamwino, mkoani Dodoma, wameuawa na wananchi wenye hasira baada ya kufanya uporaji huo.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alisema Desemba 21, mwaka huu, saa 3:00 usiku katika kijiji cha Dabalo, watu sita waliosadikiwa kuwa majambazi, walikwenda kijijini hapo wakiwa wamepakizana katika pikipiki mbili tofauti, moja ikiwa na namba T194 CQF aina ya Sunlg na nyingine haikufahamika namba.

Aliwataja waliouawa kuwa ni Jonas Chinaa mkazi wa Dakawa, Morogoro, Elias Kazembe (32) wa Ifakara mkoani Morogoro na mwingine aliyetambulika kwa jina moja la Nzungu (30 hadi 35) mkazi wa Kiteto, Manyara.

Wengine wawili waliokamatwa wakiwa hai ni Shaban Mkanange (39) mkazi wa Dumila, Morogoro na Mashaka John (26) mkazi wa Ikombo Dabalo, Chamwino ambaye alikuwa mwenyeji wao.

Kamanda Mambosasa alisema baada ya watu hao kupora kiasi hicho cha fedha, waliondoka katika eneo hilo la tukio kwa kutumia usafiri waliokwenda nao sehemu ya tukio wakiwa wamepakizana ‘mshikaki’.

Alisema baada ya kufanya uhalifu huo, taarifa zilienea kwa wananchi wa vijiji vya jirani vikiwamo vya Hombolo na Segala kisha kuanza msako kwenye mapori huku wakifunga barabara kwa kuweka vizuizi vya mawe.

Mambosasa alisema watu hao walipofika kijiji cha Segala, walikutana na kizuizi cha mawe hivyo kuamua kugeuka na kwenda katika kijiji cha Manyemba ambako huko nako walikutana na kundi la watu.

“Baada ya kuona kundi la watu, majambazi hao waliamua kufyatua risasi na kuwajeruhi Nyembela Mganga katika mguu wa kushoto na mkewe Ndalandala Nyembela mguu wa kulia, wote wakazi wa kijiji cha Manyemba ambao walipelekwa hospitalini na kutibiwa na hali zao zinaendelea vizuri,” alisema Mambosasa.

Hata hivyo, alisema baada ya watu hao kuona miale ya mianga ya tochi wakiwa wamezungukwa pande zote, waliamua kutelekeza pikipiki na kukimbilia mlima Kinyami katika kijiji cha Hombolo.

“Msako uliendelea kwa kuwajumuisha polisi wa kituo cha polisi Dabalo na wananchi hadi Desemba 22, mwaka huu, lakini walipokaribia kukamatwa, walifyatua risasi hewani kuwatisha wananchi kwa lengo la kuwatawanya,” alisema.

Kamanda Mambosasa alisema licha ya vitisho vya majambazi hao, wananchi hawakurudi nyuma hadi walipoishiwa risasi na kuanza kukimbia pande tofauti kwa lengo la kujiokoa na hasira za wananchi.

Alisema watu hao walifukuzwa na wananchi na hatimaye kukamatwa watano ambao walianza kushambuliwa kwa silaha mbalimbali za jadi hadi kuuawa papo hapo.

Mambosasa alisema watu hao pia walikamatwa na silaha tatu moja aina ya shotgun iliyofutwa namba na magobore mawili.
Mpya zaidi Nzee zaidi