Airtel yafikiria ‘kuzitema’ nchi 15

Dar es Salaam. Kampuni ya Bharti Airtel ina mpango wa kujiondoa kutoka nchi 15, ikiwamo Tanzania, baada ya kutofanya vizuri katika robo ya mwisho ya mwaka jana.

Juzi gazeti la Mwananchi liliripoti mchakato wa kupunguza wafanyakazi wa kitengo cha huduma kwa wateja huku sababu zikitolewa kuwa ni kudorora kwa biashara.

Katika kipindi hicho, imeelezwa kuwa Airtel ilipata hasara ya Sh203 bilioni kutokana na kutofanya vizuri sokoni, kulinganisha na hasara ya dola 170 milioni iliyopata mwaka jana.

Akiongea na mtandao wa habari za kiuchumi wa Bloomberg, Mwenyekiti wa Bharti inayomiliki Airtel,  Sunil Bharti Mittal alisema wameamua kuunganisha biashara au kuuza hisa zake kwenye nchi 15 za Afrika ili kulipa madeni.

“Hali ngumu ya kiuchumi imeikumba dunia, hata nchi za Marekani na China, hivyo nchi 15 za Afrika zitaathirika na mpango huu,” alisema Mittal.

Meneja uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema ameiona taarifa hiyo katika vyanzo vikubwa vya habari ila kwa Tanzania bado hawajataarifiwa.

Alisema hawezi kutolea ufafanuzi taarifa hiyo kwa kuwa ni suala la makao makuu ya kampuni hiyo, Bhatli Airtel iliyopo nchini India na kwa Afrika tawi kuu lipo Nigeria.
Mpya zaidi Nzee zaidi