Vidonda vya tumbo vyawa tatizo nchini

Dar es Salaam. Matumizi ya muda mrefu ya dawa aina ya diclofenac na diclopar yametajwa na wataalamu kuwa sehemu ya vyanzo vikuu viwili vinavyochangia ongezeko la wagonjwa wa vidonda vya tumbo nchini.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ya binadamu, tofauti na ilivyokuwa inafikiriwa awali, vidonda vya tumbo kwa sasa vimeonyesha kuwashambulia hata vijana na watoto wadogo kutokana na sababu mbalimbali.

Utafiti wa kimataifa uliochapishwa katika jarida la Saudi Journal of Gastroenterology mwaka 2009 ulioidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watu duniani wana vimelea vya bakteria wanaoambukiza ugonjwa huo, huku miongoni mwao, karibu asilimia 80 huwa hawaonyeshi dalili yoyote ya kuugua ugonjwa wa vidonda vya tumbo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Daktari wa Magonjwa ya Binadamu na Lishe wa Hospitali ya Bugando, George Kaanan alisema kuna vyanzo viwili vikuu vya vidonda vya tumbo ambavyo ni kuambukizwa kwa njia ya bakteria aina ya helicobacter pylori na kwa njia ya homoni.

Wakati Dk Kaanan akisema bakteria aitwaye helicobacter pylori ndiye huambukiza aina ya kwanza ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo, hugunduliwa kwa kutumia kipimo cha H. Pylori, aina ya pili inachangiwa na mwili kuzalisha homoni nyingi kutokana na mfumo wa maisha.
Mpya zaidi Nzee zaidi