Polisi kumsaka kisa kutoweka na funguo

KATIBU MKUU WIZARA YA NISHATI NA MADINI, PROFESA JUSTINE NTALIKWA.

KATIBU Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justine Ntalikwa, ameagiza kutumika kwa polisi katika kumsaka Mganga wa Zahanati ya Chuo cha Madini tawi la Nzega mkoani Tabora, anayedaiwa kutoweka na funguo na kusababisha watumishi na wanachuo kukosa huduma ya afya.

Alitoa agizo hilo jana kwa Bodi ya Ushauri ya chuo hicho, alipokuwa akizindua Bodi mpya ya Chuo chini ya Mwenyekiti, Profesa William Mwegoha, mjini hapa jana.

Aliitaka Bodi hiyo kutumia polisi kumsaka Mganga huyo ambaye hakumtaja jina lake, baada ya kutafutwa kwa muda mrefu bila mafanikio.

“Hatua hiyo ni lazima itumike kwani tayari mganga huyo amekwisha tafutwa kwa muda mrefu bila mafanikio, ametoweka na funguo takribani miezi mitatu,” alisema Prof. Ntalikwa.

Alifafanua kuwa kitendo hicho kinasababisha watumishi na wanafunzi kukosa huduma ya afya.

Aidha, alisema dawa alizokabidhiwa mganga huyo, lazima zihakikiwe.

Sambamba na hayo, Prof. Ntalikwa aliagiza bodi hiyo kuimarisha ulinzi katika chuo hicho ili kunusuru wizi, upotevu na uvamizi wa maeneo ya machimbo unaofanywa na wachimbaji wadogo wa madini.

“Hivi karibuni nilifanya ziara na kutembelea chuo hicho, nilikuta kipo taabani na kinahitaji msaada wa haraka kutatua changamoto zilizopo,” alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na kutokuwapo kwa ulinzi, upotevu wa vitu unaendelea kuwapo siku hadi siku.

Prof. Ntalikwa pia aliitaka Bodi kuhakikisha inatafuta kampuni ya ulinzi haraka na kufanya makubaliano ili ianze kazi hiyo mara moja.

Kadhalika, alisema Chuo kinakabiliwa na madeni ambayo wazabuni na watumishi wanakidai na kwamba kwa mwaka wa fedha 2015/16, deni lilikuwa limefikia Sh. bilioni 1.4.

Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17, anatambua kuwa walipatiwa kiasi cha fedha ambacho ni asilimia 21 tu ya bajeti, jambo ambalo limechangia washindwe kufikia malengo.

Naye Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Vincent Pazia, alisema chuo hicho chenye uwezo wa wanafunzi 200, kina wanafunzi 527 (sawa na asilimia 263 ya uwezo wake halisi), kinatoa kozi mbalimbali ikiwamo ya mafundi sanifu katika sekta za madini, mafuta na gesi ambazo zinahitajika sana kitaifa hivi sasa.

Aliongeza kuwa katika changamoto hiyo ya wingi wa wanafunzi, kila muhula mpya wa masomo, hupokea maombi mapya yasiyopungua 1,000 (sawa na asilimia 500 ya uwezo wa chuo).

Kwa mujibu wa Pazia, chuo kina matawi mawili ya Dodoma na Nzega.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, katika ufafanuzi wake alikiri mapungufu yaliyotajwa ikiwamo miundombinu duni katika matawi yote.

JIUNGE NASI KATIKA
INSTA
GRAM @Muungwanablog

FACEBOOK @Muungwana Blog

YOUTUBE @Muungwana Tube

BOFYA HAPA KU-INSTALLAPP YA MUUNGWANA BLOG ILI UPATE URAHISI KUZISOMA HABARI ZOTE KWA WAKATI.
Mpya zaidi Nzee zaidi