Bajeti yatengwa uhakiki wa mali za viongozi wa umma

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema Serikali imetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2017/18 kwa ajili ya uhakiki wa mali za viongozi.

Kairuki aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa menejimenti ya taarifa za kimaadili, alisema ifikapo Desemba 31, viongozi wa umma watajaza fomu za maadili kwa njia ya mtandao.

Desemba, mwaka jana sekretarieti ilipanga kuhakiki mali za viongozi 500, lakini walifanikiwa kuhakiki mali za viongozi 116 tu kati ya viongozi 15,824 wanaotakiwa kuhakikiwa nchi nzima ili kukidhi matakwa ya sheria.

Hata hivyo, jana, Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma ilisema imeshindwa kuhakiki mali za viongozi hao 384 kwa sababu imekosa fedha za kutosha kutekeleza jukumu hilo la kisheria.

Kamishna wa Maadili, Jaji Harold Nsekela alisema mfumo huo utatumika kuhifadhi taarifa za viongozi wa umma na malalamiko ya wananchi.

Alisema viongozi wengi bado hawajahojiwa kwa sababu idadi yao ni kubwa na sekretarieti haina fedha za kutosha kuhakiki taarifa zao.

Hata hivyo, amewaomba viongozi kutoa taarifa sahihi kuhusu mali na madeni wanayodaiwa.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items