Kamatakamata madereva malori yazindua wamiliki

CHAMA cha Wafanyakazi wa Usafirishaji kwa njia ya Barabara Tanzania (Tarotwu), kimewaonya baadhi ya madereva wa malori yanayosafirisha mizigo ndani na nje ya nchi, kwa madai kwamba wanahujumu mizigo ikiwamo kuiba mafuta.

Kutokana na hali hiyo, madereva wanne raia wa Tanzania, wanashikiliwa nchini Zambia wakituhumiwa kuiba zaidi ya lita 1,000 za mafuta na mizigo waliyosafirishwa kwenda nchini humo.

Aidha, chama hicho kimewataka wamiliki wa malori hayo kulipa mishahara madereva hao kwa wakati, posho na kuwapa mikataba ya ajira kutokana na makubaliano yao mwaka jana kati yao na iliyokuwa Wizara ya Kazi na Ajira upitia kamati ya Waziri Mkuu.

Katibu Mkuu Tarotwu, Salum Abdallah, akisoma tamko la chama hicho jijini Dar es Salaam jana, alisema chama hicho kimepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya waajiri na wamiliki wa kampuni za usafirishaji, kuhusu kuibiwa na kuhujumiwa mali ikiwamo kuangusha malori ya mafuta.

Alisema madereva hao mbali na kuaminiwa na waajiri wao na kukabidhiwa malori ya mafuta yenye lita za ujazo 35,000 wamelalamikiwa kupunguza mafuta hayo kabla ya kufikisha mzigo huo mahala husika.

“Madereva wamefanya matukio hayo mfululizo hivi karibuni na kugundua kwamba mtandao wa hujuma hizi unakua na hii itatuathiri sisi Watanzania kwa kuwa hatutaaminiwa na ajira tutapokonywa, wawekezaji katika sekta ya usafirishaji hususan mafuta, walioko nje hawatatuamini,” alisema Abdallah.

Pia alisema wafanyakazi hao watambue kwamba wao ni mabalozi wa Tanzania, hivyo kufanya vitendo vya aina hiyo kunaliletea sifa mbaya taifa.

Naye Mwenyekiti wa chama hicho, Shukuru Mlawa, alisema uchunguzi wa awali kutokana na hujuma hizo, unaonyesha kuwa baadhi ya madereva hawajalipwa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu, huku wengine wakiwa hawana ajira.

“Tunawataka wamiliki, waajiri wa kampuni hizi kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuwalipa kwa wakati ili kuwaondolea changamoto za kiuchumi, baada ya kukosa fedha kujikimu, ingawaje vitendo hivi vya wizi ni kosa la jinai na hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika” alisema Mlawa.

Alisema baadhi ya kampuni nchini, zikiwamo 300 za jijini Dar es Salaam, ni robo tatu tu ambazo zimetoa mikataba ya ajira kwa madereva wao.

Pia aliomba serikali iwadhibiti madereva na wafanyakazi wa maghala ya mafuta ili wafanye kazi kwa uadilifu na kulinda sifa na taswira ya nchi.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items