Kina Mavugo waibeba Stars

TIMU ya soka ya Taifa (Taifa Stars) imepanda nafasi 22 katika orodha ya viwango iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Kupaa kwa Tanzania kumetokana na ushindi ambao Taifa Stars iliupata katika mechi mbili za kirafiki za kimataifa ilizocheza mwezi uliopita dhidi ya wenzao wa Botswana na Burundi.

Mechi zote mbili zilifanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam na Taifa Stars ilikuwa ikiongozwa kwa mara ya kwanza na kocha mpya Mtanzania, Salum Mayanga aliyerithi mikoba ya Boniface Mkwasa.

Taifa Stars ilianza kupata ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na nahodha na mshambuliaji wake tegemeo, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji na ikaichapa Burundi magoli 2-1.

Wafungaji katika mechi dhidi ya Burundi walikuwa ni Simon Msuva wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga na Mbaraka Yusuph, mchezaji bora wa mwezi uliopita kutoka Kagera Sugar.

Katika orodha ya shirikisho hilo iliyopita, Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 157 na sasa imepaa hadi kwenye nafasi ya 135.

Brazil imeshika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Argentina, Ujerumani, Chile, Colombia, Ufaransa, Ubelgiji, Ureno, Uswisi na Hispania.

Orodha nyingine ya viwango ya shirikisho hilo itatolewa ifikapo Mei 4 mwaka huu.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items