Mizigo ya IGP Sirro haibebeki, Mangu adai hajawahi kuiona

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro atakuwa akitafakari mizigo mikubwa iliyo mbele yake baada ya kuapishwa jana.

Lililo juu kabisa ni la mauaji ya viongozi wa vijiji na askari katika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani.

Mauaji hayo ndiyo yanatajwa kuwa moja ya sababu zilizomuondoa mtangulizi wake, Ernest Mangu ambaye ameongoza Jeshi la Polisi kwa miaka mitatu na miezi sita tangu alipoteuliwa Januari Mosi, 2014.

Lakini huo hautakuwa mzigo pekee kwa Kamanda Sirro, kwa kuwa kurudi kwa ujambazi, malalamiko ya vyama vya upinzani dhidi ya matumizi ya chombo hicho kwa wanasiasa na kero za wananchi dhidi ya vitendo vya ubambikiaji ni mizigo mingine atakayobeba IGP Sirro.

Sirro ameteuliwa juzi kushika wadhifa huo akichukua nafasi ya Mangu ambaye Rais amesema atampangia kazi nyingine.

Kabla ya uteuzi huo, Sirro alikuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, pia aliwahi kuwa kamanda wa polisi wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza kabla ya kuhamishiwa Dar es Salaam kuwa Mkuu wa Operesheni na Mafunzo.

Suala la mauaji ya Kibiti na Rufiji limechukua nafasi kubwa katika mijadala ya siku za karibuni na chini ya uongozi wa Mangu, Jeshi la Polisi limeweka kambi Kibiti, lakini wauaji wameua viongozi wawili zaidi wa vijiji na vitongoji.