Dereva wa basi afariki dunia baada ya kugongana na lori

DEREVA wa basi la kampuni ya Super Feo, Ismail Nyami (38), mkazi wa Bombambili Manispaa ya Songea, amefariki dunia papo hapo baada ya basi alilokuwa akiendesha kugongana uso kwa uso na lori lenye shehena ya makaa ya mawe.

Wakati dereva huyo akipoteza maisha, abuiria 11 wamejeruhiwa vibaya na kulazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Gemini Mushy, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12 jioni katika eneo la Msalaba, kijiji cha Mbangamawe barabara ya Njombe- Songea kilomita chache kutoka Songea mjini.

Alisema basi hilo la abiria lenye namba za usajili T213 BNU aina ya Yutong, liligongana na gari lenye namba za usajili T159 CEX aina ya Iveco Stralis likiwa na tela lenye namba T206 CHS, mali ya kampuni Trank Link Limited ya jijini Dar es Salaam.

Mushy alisema basi hilo likiwa na abiria 46, lilikuwa linatoka Mbeya kwenda Songea wakati lori hilo likitoka kwenye mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka wilayani Mbinga kwenda Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kamanda Mushy, chanzo cha ajali hiyo ni mwendo mkali wa dereva wa lori uliosababisha kukosa mwelekeo na kulivamia basi hilo.

Aliwataja majeruhi kuwa ni Salome Chale (25) mkazi wa Bombambili, Winfrida Chitanda (31) mkazi wa Mbeya, Fransisca Nyari (22) mkazi wa Dar es Salaam, Irene Malisa (15) mkazi wa Mbeya, Oresto Nyoni (58) mkazi wa Matarawe Manispaa ya Songea na Noela Ndunguru (25) mkazi wa Kihungu wilayani Mbinga.

Wengine ni Anifrida Lameck (30) mkazi wa Dar es Salaam, Mariam Salehe (30) mkazi wa Mbeya, Hebron Gaitan (4) mkazi wa Vwawa mkoani Songwe, Paulina Mnimbo (25) na Joseph Elia (47) wote wakazi wa Songea mjini.

Alisema majeruhi hao wanapatiwa matibabu hospitalini hapo na kwamba sita kati yao wana hali mbaya.

Pia alisema Jeshi la Polisi mkoani hapa linamsaka dereva wa lori hilo ambaye alikimbia na kutokomea kusikojulikana baada ya ajali.